Vihoja vyatokea mahakamani Mombasa
By Munna Swaleh
Kijana aliyeshtakiwa kwa kosa la kuvuruga amani,aliieleza mahaka kuwa alifanya hivyo kulinda ndoa yake kuvunjwa na jamaa alikuwa anamyemelea mkewe.
Hassan Salim alieleza kuwa alijawa na hasira baada ya kuingia katika kibanda cha chakula kilichomilikiwa na mkewe na kumpata akimlisha Bw Jaffar Mwalimu Mwazecha.
Aidha aliiambia mahakama kuwa hiyo haikuwa mara ya kwanza kumpata mkewe akiwa katika hali hiyo na Bw Mwazecha.
“Muheshimiwa mlalamishi mbali na kujaribu kumnyemelea mke wangu aliingilia vita kati yetu,nilipomkuta mke wangu akimlisha bwana huyo nilijawa na hasira mno,”alisema.
Alieleza mahakama iliyoongozwa na hakimu mkaazi Bw Edgar Kagoni kuwa alimuomba mkewe amruhusu kumlisha mwanamume huyo jambo lililozua ugomvi kati yake na mkewe.
“Nilimuomba mke wangu anipe fursa ya kumlisha Bw Mwazecha, kwani kwa maoni yangu, nikuwa bwana huyo alipenda kulishwa,nilipojaribu kumlisha mkewangu alinishika mkono jambo lililozuwa vurugu kati yetu,ni wakati huu ambapo mlalamishi aliingilia ugomvi wetu na kunizidisha ghadhabu zaidi,”alisema.
Maelezo yaliyotolewa kortini ni kuwa Salim alishtakiwa kwa kosa la kumtishia Bw Mwazecha Maisha na kuzua rabsha ambayo ingevuruga amani.
Alidaiwa kumwambia Bw Mwazeche kuwa“We hunijui,mimi ni mbaya,ntakuulia mbali Shoga wewe,”
Mshukiwa alidaiwa kutekeleza kosa hilo mnamo Agosti 18, katika maeneo ya Msufini, Likoni katika Kaunti ya Mombasa.
Alikubali shtaka hilo.
Aliachiliwa bila dhamana na kuagizwa kurudi Kortini Septemba 3, kwa uwamuzi.
Katika Korti hiyo hiyo mwanamume mwengine aliyeshtakiwa na kosa la kutishia kuuwa,aliachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh 20,000.
Mahakama ilielezwa kuwa akiwa amejihami kwa kisu Paul Hamilton alitishia kumtoa uhai Bw Mukambe Nyawa.
Tukio lilidaiwa kutendeka Agosti 18 katika mtaa wa Tudor, Mombasa.
Alikabiliwa na shtaka jengine la kuvuruga amani.
Alikanusha mashtaka yote mawili.
Kesi itatajwa Septemba 3