Tanzania miongoni mwa mataifa 10 ya mwisho kwa viwango vya furaha duniani

Tanzania ni miongoni mwa nchi kumi za mwisho kwa viwango vya furaha kulingana na ripoti ya Viwango vya Furaha Duniani ya mwaka 2016.

Orodha hiyo iliandaliwa kwa kuangazia pato la mtu kwa kila mwaka,miaka ambayo mtu anatarajiwa kuishi, kuwa na mtu wa kutegemea kwa usaidizi, dhana ya kuwepo uhuru wa kufanya maamuzi maishani, uhuru kutoka kwa ufisadi, na ukarimu miongoni mwa mengine.

Mataifa yaliyo kwenye kundi la mataifa kumi ya mwisho ni Madagascar, Tanzania, Liberia, Guinea, Rwanda, Benin, Afghanistan, Togo, Syria huku Burundi ikishika mkia.

Tanzania imo nambari 149 kati ya nchi 157 ikiwa na alama 3.695 kati ya alama 10 na Rwanda nambari 152 na alama 3.315.

Uganda,nambari 146 na alama 3.739, Malawi nambari 132 na alama 4.156, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imo nambari 125 na alama 4.272 na Kenya nambari 122 na alama 4.356.

Somalia imeibuka nambari 76 na alama 5.44.

Ripoti hiyo imetolewa mjini Roma,Italia huku ulimwengu ukijiandaa kuadhimisha Siku ya Furaha Duniani ya Umoja wa Mataifa tarehe 20 Machi.

Orodha hiyo imetayarishwa na shirika la maendeleo endelevu ya Sustainable Development Solutions Network (SDSN) ambalo lilianzishwa na Umoja wa Mataifa.

Denmark inaongoza kwa viwango vya furaha duniani ikiwa na alama 7.526 ikifuatwa kwa karibu na Uswizi, Iceland na Norway.

Finland, Canada, Uholanz, New Zealand, Australia na Sweden zinafunga kumi bora.

Marekani imo nambari 13 na Uingereza nambari 23.