Hatua ya Saudia kuitolea Qatar vikwazo yapongezwa

Viongozi wa KEMNAC na ALMADA katika hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano kati yao

Mwenyekiti wa baraza la kitaifa la kutoa ushauri kwa waislamu nchini Kenya KEMNAC Sheikh Juma Ngao amepongeza hatua ya nchi ya Saudi Arabia kuitolea nchi ya Qatar vikwazo vya kidiplomasia,kibiashara na usafiri.Amesema kuwa hatua hiyo itapelekea kustawi kwa uchumi baina ya nchi hizo mbili.

Makubaliano hayo yanaashiria kufunguliwa kwa safari za ndege, mipaka na bahari kati ya Saudi Arabia na Qatar.

Ngao amezitaka nchi za Misri,Bahrain na Falme za Kiarabu kufuata mkondo wa Saudia na kutoa vikwazo kwa Qatar.

Mzozo wa kidiplomasia ulianza mnamo 2017 wakati Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri zilipokata uhusiano wa kidiplomasia, biashara na usafiri na Qatar.

Nchi hizo nne zilishutumu Qatar kwa kuunga mkono ugaidi, shutuma ambazo zilikanushwa na Qatar.

Vilevile,Ngao ameshukuru nchi za Kuwait,Uturuki na Iran kwa kusimama na Qatar wakati huo mgumu kwani hawakuiekea nchi hiyo vikwazo.

Mwenyekiti huyo ameelezea kukosekana kwa umoja kati ya nchi za kiarabu na nchi za kiislamu umechangia kuporomoka kiuchumi pamoja na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwenye nchi hizo. Hali hiyo inasababisha raia wengi kutoka nchi za kiislamu na kiarabu kuhamia mataifa ya magharibi, vilevile nchi za magharibi haswa Marekani na washirika wake, wanaendelea kukandamiza nchi za kiislamu na nchi za kiarabu.

Aidha, Ngao ametoa wito kwa Yemen na Syria kusitisha vita akitaka suluhu ya kudumu kupatikana ili kutatua chuki iliyopo kati ya nchi za kiislamu na Iran.