Wakaazi wa Jomvu wafaidika na mradi wa maji safi.

Ni afueni sasa kwa wakaazi wa Mwamlai na Chamunyu eneo bunge la Jomvu kaunti ya Mombasa baada ya serikali ya kaunti kuzindua rasmi mradi wa maji unaolenga kumaliza shida ya ukosefu wa maji safi katika maeneo hayo.
Akiongea wakati wa uzinduzi huo Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassiir amesema zaidi ya nyumba 900 zinatarajiwa kufaidika na mradi huo wa maji huku akiwarai wahusika kuondoa ada ya kuunganisha maji safi ili wakaazi wengi zaidi wafaidike na mradi huo.
Kulingana na Nassir ada inayotozwa imekuwa kikwazo kwa wakazi wengi kukosa maji safi kutokana na kushindwa kumudu gharama.
Waziri wa maji,mali asili na mabadiliko ya tabia nchi katika kaunti ya Mombasa Emmilly Achieng ameahidi kujizatiti kuhakikisha wanafikia malengo ya kusambaza maji safi kwa kila mtu ili kumaliza dhiki ambazo wananchi wanapitia kutokana na uhaba wa maji, huku akiwarai wananchi kukoma kuharibu miundo msingi ya maji ili kuhakikisha upatikanaji wa maji muda wowote.
Naye mwenyekiti ya kampuni ya usambazaji maji Selina Maitha ameahidi kushirikiana na viongozi mbalimbali kuhakikisha wakaazi wa Mombasa wamepata maji safi katika majumba yao.
Kwa upande wao wakaazi wa maeneo hayo hawakuficha furaha yao kutokana na mradi huo wakisema umewauepushia dhiki na mateso ambayo wamekuwa wakipitia kutafuta maji saf, wakiishukuru Serikali kaunti ya Mombasa kwa kutatua swala hilo la kero la maji safi.
Haya yanajiri kibainika kuwa kati ya nyumba 900 ambazo zinatarajiwa kufaidika na mradi huo katika maeneo hayo, nyumba 450 ndizo zimefanyiwa maombi ya kuunganishiwa maji huku nyumba 120 zikiwa tayari zimeunganishiwa maji na zimeanza kufaidika na mradi huo, na nyumba zilizosalia zikitarajiwa kufanikishiwa huduma hizo.