Kesi ya kupinga ushindi wa Museveni kusikizwa Jumatatu

Kesi ya kupinga ushindi wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni katika uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi uliopita inatarajiwa kusikizwa siku ya Jumatatu.
Uamuzi huo umetolewa baada ya kufanyika kwa kikao cha maandalizi ya kesi ambacho kwa mara ya kwanza kimewakutanisha majaji na mawakili wa pande zote.
Kesi hiyo iliyowasilishwa na waziri mkuu wa zamani nchini humo Amama Mbabazi katika mahakama ya juu nchini humo inahusisha mawakili zaidi ya 100.
Mbabazi, aliyeibuka wa tatu kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi, amesema kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki na hivyo anataka kura zihesabiwe tena.
Kwenye nyaraka zao za kesi, mawakili wa Mbabazi wanasema wakati wa kutangazwa kwa matokeo kulikuwa na kura 1.8 milioni ambazo hazikuwa zimehesabiwa.
Mgombea wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC) Dkt Kizza Besigye, aliyemaliza wa pili, hakufanikiwa kuwasilisha kesi ya kupinga uchaguzi wa Rais Museveni katika muda ulioruhusiwa ingawa alikuwa ametangaza kwamba hakukubali matokeo hayo.
Kesi hiyo ya Mbabazi inasikizwa na majaji tisa ambao wana muda wa siku 30 kuisikiza na kutoa uamuzi.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi nchini Uganda,Museveni alipata asilimia 60.7 ya kura, Dkt Besigye asilimia 35.4 na Mbabazi asilimia 1.39.