UN yatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano Jeber Marra,Sudan

 marta_ruedas

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano katika eneo la Jeber Marra nchini Sudan na kuruhusu mashirika ya Umoja huo kuwafikia maelfu ya watu waliokimbia mapigano.

Mratibu wa misaada ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan,Marta Ruedas amesema kuwa mapambano yanatakiwa kusimamishwa ili kuwafikishia msaada watu elfu 85 katika jimbo la Darfur Kaskazini waliokimbia makaazi yao kutokana na mapigano kwenye eneo la Jebel Marra.

Hata hivyo amesema idadi hiyo sio kamili kwa kuwa watu bado wanaendelea kukimbia mapigano.

Wakati huo huo afisi ya uratibu wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA imesema mashirika mbalimbali yameanza kutoa misaada, lakini ujio mkubwa wa wakimbizi unaleta changamoto kwenye shughuli za ugavi.