Marekani yashambulia kambi ya Islamic State Libya

Maafisa wa Marekani wamethibitisha kuwa ni ndege za Marekani zilizofanya mashambulio huko Libya wakiwalenga wanamgambo wa IS.
Hata hivyo shambulio hilo la karibu na mji wa Sabratha,lililonuiwa kumlenga hasa mpiganaji mmoja wa Tunisia limeripotiwa kuwauwa watu 30 .
Mpiganaji huyo wa Tunisia anadaiwa kufanya shambulio la mwaka jana katika kumbukumbu za Bardo na hoteli ya ufuoni mwa bahari ya Sousse,Tunisia ambako watu zaidi ya 10 waliuawa.
Kulingana na maafisa wa Marekani ni kuwa mashambulio hayo yalilenga kambi moja ya wapiganaji wa Islamic State na kumuua kiongozi mmoja mwenye itikadi kali.
Kundi la IS limekuwa likifanya oparesheni zake nchini Libya kwa kipindi cha mwaka mmoja na Marekani inakadiria kwamba lina hadi wapiganaji 6,000 nchini humo.
Libya inasalia katika machafuko ya wenyewe kwa wenyewe miaka minne baada ya kupinduliwa kwa aliyekuwa kiongozi wake Muammar Gaddafi,na inapiganiwa na makundi tofauti ikiwemo kundi la IS.