Mbunge wa Mvita asihi wakaazi wa eneo bunge hilo kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa
Huku zikiwa zimesalia siku mbili pekee kukamilika kwa zoezi la kuhesabu watu hapa nchini Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir amehimiza jamii ya eneo mbunge la Mvita kujitokeza kwenye zoezi la kuhesabu watu linaloendelea kote nchini.
Akizungumza wakati akipeana hundi ya shilingi milioni 7.8 za Uwezo Fund kwa vikundi mbali mbali hapa Mombasa, Abdulswamad amelitaja eneo bunge la mvita kama lenye idadi ndogo ya watu huku akiwataka wakaazi eneo hilo kuacha fikira potofu kuhusu zoezi hilo badala yake kujitokeza kwa wingi ili kuhesabiwa.
Aidha amedokeza kuwa iwapo wakaazi wa eneo hilo hawatajitokeza kwa wingi kwenye zoezi basi huenda baadhi ya sehemu za uwakilishi nchini zikazimwa.
Vile vile amesema kuwa zoezi hilo ni muhimu mno kote ulimwenguni kwani husaidia taifa kupanga mikakati ya wananchi wake kimaendeleo.
Amekariri kuwa taifa haliwezi kujua pahali linaeleke pasi na kujua pahali litokapo hivyo basi ni sharti zoezi hilo lichukuliwe kwa uzito ili kuongeza kiwango Cha mgao wa pato la kitaifa kwa kila eneo bunge nchini.