Mzozo wa ardhi Kilifi waibuka
By Noah Mwachiro
Zaidi ya wakazi alfu 50 katika eneo la Chonyi kaunti ndogo ya Kilifi Kusini wanaishi kwa hofu ya kuvunjiwa nyumba zao baada ya bwenyenye mmoja kujitokeza na kudai umiliki wa ardhi yao ya ekari 1700.
Wakazi hao kutoka eneo la Kayole, Dindiri na Makata wanasema Bwenyenye huyo kwa Jina Islam Mubarakh Abeid anadai kutoka katika familia ya Mazurui na ana hati miliki ya shamba hilo ya tangu mwaka 1902.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi mwenyekiti wa kamati ya ardhi ya eneo hilo Ronald Muzika amesema hawawezi kukubali kuondoka katika ardhi hiyo kwani wamekuwepo kwa zaidi ya miaka mia moja na wanavyojua ni kwamba katiba ilizifutilia mbali hati miliki za ardhi za wakati wa mkoloni.
Kulingana na Tobbias Chigiri mweka hazina wa kamati hiyo juhudi zao za kuwahusisha viongozi wa utawala zimeambulia patupu kwani viongozi hao wameonekana kuungana na bwenyenye huyo.
Wazee hao wameyataka mashirika ya kutetea haki za kibinadam kuwasaidia kwani wamekuwa wakipokea vitisho vya kuuwawa kutoka kwa watu wasiojulikana.
Tukiachana na hofu hii inayoshuhudiwa eneo la Chonyi, mzozo wa ardhi ya ekari ishirini na moja unazidi kutokota baina ya familia moja na mabwenyenye katika eneo la Mwendo wa Panya Kanamai Kaunti ya Kilifi.
Ikiongozwa na Zainab Mohamed Hathor, familia hiyo imesema licha ya kuishi kwenye kipande hicho kwa muda wa miaka mingi sasa mabwenyenye hao wamekuwa wakiwahangaisha.
Wanasema mimea yao ikiwamo minazi imeharibiwa kwa kukatwa na mabwenyenye hao huku baadhi ya vipande vya ardhi hiyo vikiwa tayari vimeuzwa.
Wametaja kuishi kwa hofu baada ya mabwenyenye hao kuwatishia maisha huku wakimshinikiza rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati mzozo huo.
Suala la utata wa ardi limekuwa donga sugu kaunti ya Kilifi huku wananchi wengi wakisalia kuhangaika baada ya kukithiri kwa uvunjaji wa nyumba zao na mabwenyenye chini ya usimamizi wa maafisa wa usalama .
Kwa sasa takriban nusu ya ardhi ya kaunti ya Kilifi inakubwa na utata kuanzia sehemu za Mtwapa,Chonyi,Ganze, Magarini na sehemu nyinginezo huku juhudi za viongozi wa kisiasa zikionekana kutozaa matunda, Swali likiwa ni je ni nani atakaye wakomboa wakazi wa Kilifi?