Tume ya EACC yabainisha kuwa kesi 120 za ufisadi kanda ya pwani zimewasilishwa Mahakamani
TUME ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC imedokeza kuwa imewasilisha jumla ya kesi 120 katika mahakama mbalimbali kanda ya pwani ambapo inalenga kuregesha mali ya umma ya thamani ya shilingi bilioni 8 kwa ujumla katika eneo hilo.
Mali hizo zinasemekana kupatikana kwa njia za ulaghai na hivi sasa ziko chini ya umiliki wa watu binafsi, huku kaunti ya Mombasa ikitajwa kuongoza kwa visa vya unyakuzi wa ardhi katika kanda ya pwani.
Mali zilizonyakuliwa zinajumuisha vipande vya ardhi na majengo ya serikali yanayomilikiwa na taasisi za umma.
Miongoni mwa kesi zilizowasilishwa mahakamani ni ile inayohusu unyakuzi wa ardhi ya umma ya thamani Shilingi bilioni 2 inayomilikiwa na halmashauri ya viwanja vya ndege nchini KAA ambayo ilikuwa imetegwa kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa kimataifa wa ndege wa Moi.
kesi nyengine ni ile inayohusu kuchukuliwa kinyume cha Sharia kwa majengo ya makaazi ya wafanyikazi wa halmashauri ukusanyaji wa mapato nchini KRA yanayokadiriwa kuwa na thamani ya Shilingi 358.5, miongoni mwa kesi nyengine.
kulingana na afisa mkuu wa mawasiliano katika tume ya EACC Erick Ngumbi,tume hiyo imekuwa ikitumia mikakati mbalimbali kufanya uchunguzi wa mali zinazomilikiwa na maafisa wa umma serikalini ili kubainisha iwapo wamezipata kwa kwa njia halali au la.
Amesema kupitia mikakati hiyo, ndani ya kipindi cha miaka minne iliyopita tume ya EACC imepata mafanikio makubwa kwani imeweza kuregesha jumla ya Shilingi bilioni 23.7 zilizokuwa zimefisadiwa.
Wakati huo huo ameyarai mashirika yanayojukumika kulinda za umma kuwajibikia majukumu yao ipasavyo kwani amedokeza kuwa uchunguzi waliyoufanya umebainisha kuwa baadhi ya maafisa wa ardhi kwenye kaunti mbalimbali wamekuwa wakishirikiana na wanyakuzi kutekeleza vitendo vya ulaghai.