EACC yapinga marekebisho ya mswada wa sheria dhidi ya ufisadi
Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC imepinga pendekezo la kufanyiwa marekebisho mswada kuhusu vita dhidi ya ufisadi nchini unaoshinikizwa na mbunge wa Mbeere Kaskazini Geoffrey Ruku.
Kulingana na naibu afisa mkuu wa tume hiyo Abdi Muhamud hatua hiyo itafungua mianya zaidi ya kashfa kubwa za ufisadi katika mashirika ya serikali na kueregesha nyuma hatua zilizopigwa na tume hiyo katika vita dhidi ya ufisadi nchini.
Abdi ameyasema hayo kwenye kaunti ya Mombasa wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku tano inayowaleta pamoja maafisa watoaji zabuni na kusimamia ununuzi katika serikali ya kitaifa na zile za kaunti nchini katika kujadili mbinu muafaka za ushirikiano ili kukabiliana na tatizo hilo.
Aidha naibu afisa huyo mkuu amedokeza kuwa tume ya EACC inaendeleza uchunguzi kuhusiana na kashfa ya utolewaji za zabuni katika taasisi Kemsa pamoja na serikali ya kaunti ya Siaya ambapo takriban shilingi bilioni moja zinasemekana kufujwa.
Wakati huo huo amebaibisha kuwa asilimia themanini ya visa vya ufisadi serikalini vinachangiwa na maafisa wa utoaji wa zabuni na ununuzi wa bidhaa serikalini huku akibainisha kuwa mikakati muafaka tayari imewekwa ili kuhakikisha kuwa mali zote za umma zilizofujwa zinaregeshwa sawia na kushtakiwa kwa maafisa wa serikali watakaopatika kuhusika na kashfa hizo.
Kwa upande wake John Karani mwenyekiti kutoka wa taasisi ya kitaifa kusimamia usambazwaji amesema kuwa warsha hiyo itawasaidia maafisa wa wanaotoa zabuni katika serikali ya kitaifa na zile za kaunti kuhamasishwa kimalifu kuhusiana na utendakazi bora wa majukumu yao.