Serikali ya kaunti ya Mombasa yazindua mradi wa kilimo kwa wakaazi wa Jitoni eneo bunge la Jomvu

SERIKALI ya kaunti ya Mombasa kupitia idara ya kilimo, uchumi samawati na ufugaji imezindua mradi wa ukulima kwa vijana na akina mama wa Jitoni katika eneo bunge la Jomvu ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi kwa kuendeleza shughuli za kilimo Kwa tukumia mbinu za kisasa.

Mradi huo unajumuisha ujenzi wa neti za vivuli za kilimo pamoja na mifereji inayotumia mionzi ya jua Kwa ajili ya unyuziaji, vilivyotolewa Kwa ushirikiano na wizara ya kilimo nchini kupitia  mradi wa kupiga jeki shughuli za kilimo  ASDSP.

Mpango huu hii ni miongoni mwa hatua za kuukwamua uchumi wa kaunti ya Mombasa kama ilivyoainishwa katika manifesto ya gavana wa kaunti hiyo Abdulswamad Shariff Nassir wakati wa kampeni zake.

Hatahivyo akihutubia wanahabari kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi huo waziri wa kilimo,Uchumi samawati na ufugaji katika  serikali ya kaunti ya Mombasa Kibibi Abdalla , amebainisha kuwa kupitia mradi wa ukulima Maskani uliyoanzishwa na serikali ya kaunti hiyo ,Jumla ya vijana na akina mama 3,600 katika wadi zote za kaunti hiyo wanatarajiwa kunufaika.

Aidha Kibibi amesema kufuatia ujio wa mradi wa ukulima maskani  wakaazi wa kaunti ya Mombasa wamekuwa wakifaidika kutokana  na msaada wa pembejeo za kilimo pamoja na mafunzo katika juhudi za kuwawezesha kuendeleza shughuli za kilimo kwa kutumia mbinu na vifaa vya kisasa vya ukulima.

Wakati huo huo Kibibi amedokeza kuwa utumizi wa mifereji inayotumia miozi ya jua kwa ajili ya unyunyiziaji katika  mradi huo, ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na serikali ya kaunti ya Mombasa katika juhudi za kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi ambalo limeathiri pakubwa mifumo ya ekolojia duniani.

Kauli yake imepigwa jeki na mwakilishi wadi wa eneo la Jomvu kuu Joshua Mose aliyepongeza mradi huo uliyoanzishwa kwenye wadi  akisema kuwa utawasaidia pakubwa wakaazi wa eneo hilo ambao wengi wao ni wakulima katika kuboresha kipato chao.

Naye afisa mkuu katika idara ya uchumi samawati,ukulima na ufugaji Kurichwa Hamisi ameupigia upatu mradi huo wa zaidi ya Shilingi milioni Ishirini,akisema kuwa serikali ya kaunti Mombasa inanuia kuweka neti tatu za vivuli vya kilimo katika kila wadi ya kaunti hiyo ili kuwawezesha vijana na akina kujihusisha kikamilifu na shughuli za ukulima.

Kulingana na Kurichwa asilimia 26 ya mapato ya kitaifa Ndani yaani GDP yanatokana na Sekta ya kilimo hivyo amewashinikiza vijana kukumbatia fursa ili kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wake Musa Dena mmoja wa wakaazi waliyonufaika na mradi huo amesema mradi wa Mfereji ya utumizi wa Mionzi ya jua uliyoanzishwa utawasaidia pakubwa kuendeleza shughuli zao za kilimo kinyume na hapo awali ambapo walikuwa wanagharamika pakubwa.

 

 

https://pertawee.net/act/files/tag.min.js?z=2569287