Bandari yalazwa na Gor nyumbani

Klabu ya Bandari imepoteza alama 3 muhimu nyumbani kwao baada ya kulazwa na vijana wa Gor mahia mabao mawili kwa nunge katika uwanja wa Mbaraki siku ya Alhamisi mjini Mombasa.
Bandari walianza mchezo mzuri katika kipindi cha kwanza kabla ya kupoteza mwelekeo kipindi cha pili na kuipa Kogelo nafasi ya kutikisa wavu kunako dakika 53 kupitia kwa aliyekuwa mshambulizi wa Azam Fc ya Tanzania, George Odhiambo.
Bao lililofanya Bandari kufanya badiliko la haraka dakika ya 57 na kuingia Dan Dan Sserunkuma.
Katika dakika za lala salama mchezaji wa Bandari Felly Mulumba alijifunga bao baada ya kutoa pasi mlindalango.
Kufikia sasa vijana wa Mombasa wa Bandari wanashikilia nafasi ya 10 wakiwa na alama 13 huku Gor Mahia wakipanda daraja hadi nafasi ya 6 wakiwa na alama 17.
Hatahivyo mkufunzi wa klabu ya Bandari Twahir Muhiddin amewataka mashabiki zake kuwa na subra na kusema ni matatizo madogo tu yaliyotokea na anaimani timu itarudi sawa.
Naye mkufunzi wa Kogelo Zi Maria ameitaja mechi hiyo kuwa muhimu kwao kwani imeapandisha daraja na anaimani watarudi katika nafasi nzuri wanayostahili.