Kidero afutilia mbali leseni za uegeshaji matatu jijini Nairobi

 

Gavana wa kaunti ya Nairobi Evans Kidero amefutilia mbali leseni za uegeshaji wa matatu katikati mwa jiji la Nairobi kufuatia maandamano ya wafanyibiashara waliotishia kutolipa ushuru.

Wafanyibiashara walitishia kutolipa kodi katika baraza la kaunti ya Nairobi kwa madai kwamba matatu zinaegesha magari yao mbele ya bidhaa zao na kutatiza shughuli za biashara yao.

Kidero amesema kuongezeka kwa utovu wa nidhamu kwa wenye matatu kumeathiri biashara kati kati ya jiji na ameagiza idara husika kuanza kutoa leseni hizo upya.

Akizungumza katika hafla ya kumwapisha waziri mpya wa mazingira,maji na usafi Peter Kimori,Kidero amesema hatua hiyo pia itasaidia kuondoa msongamano wa magari katikati mwa jiji.