Kijana akatwakatwa kwa panga na kutupwa msituni

 

Wakazi wa kijiji cha Mida wilayani Malindi kaunti ya Kilifi wameamkia tukio la kustaajabisha asubuhi hii baada ya kumpata kijana mmoja ameuwawa kwa kukatwa katwa kwa silaha inayoaminika kuwa panga.

Naibu chifu wa kata ya Mida Renson Baya amesema mwili wa marehemu Karisa Karani mwenye umri wa miaka 30 umepatikana kwenye msitu wa Arabuko Sokoke ukiwa umetupwa na watu wasiojulikana baada ya kisa hicho kutendeka.

Baya amesema mwendazake alikuwa akifanya kazi kwenye kibanda cha MPESA katika eneo hilo na kwamba ni mkaazi wa eneo la Malanga.

Polisi waliofika mahali hapo wamepata kijibarua kilichoandikwa kuwa” BIBI YA MTU NI SUMU ” kwenye mgongo wake huku ikidaiwa kuwa huenda alishambuliwa kutokana na tuhuma za kushiriki mapenzi na bibi ya wenyewe.

Mwili wa mwendazake umepelekwa kwenye hifadhi ya hospitali ya wilaya ya Malindi huku uchunguzi ukiwa unaendelea kubaini kilichosababisha kifo hicho.