Bendtner apigwa faini kwa kuchelewa kufika mazoezini

 

Mshambulizi wa klabu ya Wolfsburg ya Ujerumani Nicklas Bendtner amepigwa faini baada ya kuchelewa kufika mazoezini kwa sababu ya kulala kupita kiasi.

Bendtner, raia wa Denmark ambaye aliwahi kuichezea Arsenal ya Uingereza, alichelewa kwa dakika 45 baada ya kukosa kusikia mlio wa kengele ya saa ya kumuamsha.

Sasa Wolfsburg imempiga faini ya euro 2,250 ikiwa ni uro 50 kwa kila dakika aliyochelewa.

Mwezi jana,Bendtner mwenye umri wa miaka 28 aliadhibiwa baada ya kuweka mtandaoni picha akiwa na gari lake la Mercedes kinyume cha sheria za Wolfsburg zinazowaruhusu wachezaji na wakufunzi kutumia magari ya Volkswagen pekee wakielekea mazoezini.

Pia aliwahi kupigwa faini ya £80,000 na kupigwa marufuku mechi moja na Uefa baada ya kufichua suruali ya ndani yenye nembo ya mdhamini baada ya kufunga bao dhidi ya Ureno Euro 2012.

Pia alitozwa faini na Arsenal mwaka 2014 kwa kwenda Copenhagen bila idhini.