Harambee Stars tayari kwa michuano nchini Guinea Bissau asema Okumbi

Timu ya taifa ya soka Harambee Stars itaondoka nchini Jumapili hii kuelekea nchini Guinea Bissau kuchuana na wenyeji wao katika mechi ya awamu ya kwanza kuwania kufuzu ubingwa wa Afrika mwaka kesho.
Kocha Stanley Okumbi amesema vijana wake wamejiandaa kwa mechi hiyo ambayo itakua yake ya kwanza tangu kuteuliwa kuchukua mahala pa mtangulizi wake Bobby Williamson.
Kikosi cha wachezaji 26 wanaoshiriki soka ya nyumbani kinaendelea na mazoezi yake kwa sasa ugani Kasarani jijini Nairobi.
Kikosi hicho kitapunguzwa kutoka wachezaji 26 hadi 11 ili kutoa nafasi kwa wachezaji 9 wanaocheza soka nje ya taifa la Kenya ambao wameitwa kikosini.
Aidha Okumbi amesema kiungo wa klabu ya Southmpton atasalia kuwa nahodha wa Stars chini ya uongozi wake.
Stars inahitaji ushindi katika mechi hiyo ili kujipa matumaini ya kufuzu baada yake kukosa kupata ushindi katika mechi mbili ambazo wamecheza tayari wakitoka sare dhidi ya Congo na kupoteza dhidi ya Zambia.