Wizara ya usalama wa ndani yaongoza kwa ufisadi utafiti waonyesha

Utafiti mpya uliofanywa na tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC unaonyesha kuwa wizara ya usalama wa ndani ndio inaongoza kwa ufisadi nchini kwa asilimia 40.3.
Utafiti huo umeonyesha kuwa wizara ya afya ni ya pili kwa viwango vya ufisadi kwa aslimia 14.3 na wizara ya ardhi ni ya tatu kwa asilimia 11.3.
Aidha utafiti huo umeonyesha kuwa kaunti ya Murang’a ndio ya kwanza katika visa vya ufisadi ikifuatiwa na kaunti za Embu na Bometi katika nafasi za pili na tatu mtawalia.
Utafiti huo umetolewa na mkurugenzi wa utafiti na maendeleo wa EACC Nancy Namenge kwenye hafla iliyohudhuruwa na mkurugenzi mkuu wa tume hiyo Halake Wako na mwenyekiti Philip Kinusu.
Wako amesema vita dhidi ya ufisadi humu nchini havijafaulu kwa sababu ya msukumo wa kisiasa na uoga wa kufanyiwa maovu.
Utafiti huo aidha umeonyesha kuwa wakenya hutoa hongo sana wakati wa kutaka huduma za matibabu ukiwa na asilimia 20.7, kutafuta vitambulisho ikiwa na asilimia 18.4 na kutafuta cheti cha kuzaliwa ikiwa na asilimia 10.2.
Aidha idara ya polisi imetajwa kushuhudia visa vya ufisadi ikifuatwa na idara ya trafiki na afisi za chifu,idara ya mahakama na hospitali za umma mtawalia.
Hata hivyo mkuu wa sheria Githu Muigai amesema Kenya imepiga hatua katika kukabiliana na ufisadi japo bado wananchi wanaamini kwamba bado janga hilo linazidi kuwa tishio kwa hali ya maisha ya baadaye.
Sakata za kupotea kwa shilingi milioni 791 za shirika la huduma kwa vijana NYS na zaidi ya shilingi milioni 180 za mikopo kwa vijana ni baadhi ya zile ambazo Wakenya wanasema zinaleta taswira mbaya kuhusu taifa.