562,000 wajitokeza kujisajili kama wapiga kura tangu zoezi hilo kuanza

Takriban wakenya 562,000 wamejisajili kuwa wapiga kura wakati zoezi hilo linapokamilisha wiki yake ya pili tangu kung’oa nanga kote nchini.
Katika wiki ya pili wakenya 310,000 walijitokeza kushiriki zoezi hilo ikilinganishwa na idadi ya 251,000 katika wiki ya kwanza ya zoezi hilo.
Kulingana na afisa mkuu mtendaji wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC Ezra Chiloba, hatua hiyo imepelekea ongezeko la watu 58,406 kutoka wiki ya kwanza.
Hata hivyo idadi hii bado haijaafikia kiwango walichoweka tume ya uchaguzi cha kusajili wapiga kura takriban milioni mbili kufikia wiki ya pili.
Chiloba ameongeza kuwa tume hiyo ingali inafuatilia madai ya kuwahamisha wakenya wanaojisajili katika maeneo tofauti, huku akisema kuwa ripoti hiyo itatolewa maramoja pindi uchunguzi utakapo kamilika.
Zoezi hilo la siku 30 lililong’oa nanga tarehe 15 mwezi uliopita, litakamilika tarehe 15 ya mwezi huu.