Bunge la kaunti ya Embu lamtimua tena Gavana Martin Wambora
Gavana wa Embu Martin Wambora ameondolewa tena na bunge la kaunti kwa mara ya pili licha ya mahakama kulizuia bunge la kaunti hiyo kuendelea na mjadala kuhusu kuondolewa kwake.
Wajumbe 23 wa bunge la kaunti wamepiga kura kuunga mkono hoja ya kutokuwa na imani na gavana Wmbora huku nane pekee wakipinga hoja hiyo.
Wambora hata hivyo alikuwa amewasilisha kesi kupinga jaribio hilo la pili la bunge la kaunti hiyo kumuondoa madarakani.
Jaji Hedwig Ongudi ametoa agizo kuwa bunge hilo lisijadili hoja hiyo hadi pale kesi hiyo itakapo amuliwa.
Wambora anatuhumiwa kwa utumiaji mbaya wa mamlaka, na aliregeshwa madarakani na mahakama kuu licha ya kutimuliwa na bunge la kaunti pamoja na lile la seneti.
Hayo yakijiri wenyeji wa Embu wameandamana na kuwasilisha sahihi zao zaidi ya elfu 30 kumtaka rais Uhuru Kenyatta kulivunja bunge la kaunti ya Embu na serikali ya kaunti, kutokana na kile walichodeai ni kushindwa kutekeleza majukumu yake.