Awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba za kisasa za Buxton kukamilika karibuni

AWAMU ya Kwanza ya Ujenzi wa nyumba za kisasa za bei nafuu katika Eneo Buxton kwenye kaunti ya Mombasa unakaribia kukamilika,huku baadhi ya wakaazi waliyonunua nyumba hizo wakitarajiwa kukongamana mnamo siku ya Jumamosi kwa ajili ya upanzi wa miti kwenye nyumba zao.
Kulingana na Mkurugenzi mkuu wa Mradi huo Ahmed Badawy hatua hiyo ni miongoni mwa matayarisho ya kukabidhi nyumba hizo za kisasa kwa wamiliki wake na kuwa itasaidia pakubwa kuboresha mazingira ya eneo hilo sawia na kuunga mkono jitihada za serikali ya kitaifa ya upanzi wa miti bilioni tano nchini.
Aidha Badawy amesema kuwa ujenzi wa nyumba 1,300 za awamu ya pili ya mradi huo unatarajiwa kuanza hivi karibuni huku akidokeza kuwa tayari zoezi la ununuzi wa nyumba hizo limeng’oa nanga.
Itakumbukwa kuwa mradi huo ulianzishwa kama sehemu ya serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na serikali za kaunti pamoja na makampuni ya kibinafsi kuwezesha wananchi wenye mapato ya chini kumiliki nyumba nadhifu.