Kongamano la sayansi la kila mwaka laandaliwa jijini Mombasa
MUUNGANO wa madaktari wa watoto nchini KPA,umeandaa kongamano la kila Mwaka la Sayansi kwenye kaunti ya Mombasa linalonuia kuangazia athari za mabadiliko ya tabia nchi na mazingira katika afya za watoto.
Kongamano hilo aidha linalenga kutathmini kwa kina kuhusu sababu mbalimbali zinazochangia mabadiliko ya tabia nchi na kutoa suluhu muafaka.
Akihutubia wanahabari wakati wa kongamano hilo mwenyekiti wa kitaifa wa muungano huo Lawrence Okong’o amedokeza kuwa milipuko ya magonjwa pamoja na mafuriko yanayoshuhudiwa nchini, kufuatia mabadiliko ya tabia nchi,imewaathiri pakubwa watoto, hivyo ametoa wito wa kuwekwa kwa mikakati mahususi ya kudhibiti majanga hayo ili kuwalinda watoto.
Kadhalika Okong’o amedokeza kuwa muungano huo umekuwa ukiunga mkono juhudi za watunga Sera nchini kubuni sheria za kuwalinda watoto dhidi ya majanga yanayosabaishwa na mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na kushirikiana na wadau wengine kutoka mashirika ya kimataifa kuangazia kikamilifu maslahi ya watoto.
Kauli yake imeungwa mkono na afisa kutoka shirika la watoto duniani UNICEF Laura Oyiengo ambaye ameirai serikali ya Kenya kudhibiti hewa ya kaboni sawia na kutoa elimu kwa watoto kuhusiana na matumizi ya nishati safi na uhifadhi wa mazingira.
Aidha Wadau wengine wanaohudhuria kongamano hilo wametaja Mabadiliko ya Tabia nchi kuathiri ujauzito miongoni mwa wanawake hivyo kusababisha watoto wanaozaliwa kuwa na magonjwa.
Wakati huo huo wameleeza kusikitishwa na jinsi watu ulimwenguni wamekuwa wakimaliza raslimali zilizopo bila ya kujali vizazi vijavyo.