Maelfu wawasili Nairobi kwa mkutano wa Cord

Baba's returnMaelfu  ya wafuasi wa Muungano wa Cord wamewasili katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi, kwa mkutano wa kumkaribisha kinara wa muungano huo Raila Odinga ambaye anatarajiwa kuwasili baadaye leo.

Viongozi wa Muungano huo watamlaki Raila ambaye amekuwa ziarani Marekani, katika uwanja wa ndege wa kimataifa JommoKenyatta mwendo wa saa saba mchana.
Mapema leo baadhi ya wafuasi wa muungano huo wameonekana katika barabara za jiji la Nairobi huku wengine wakijumuika katika sanamu la Tom Mboya wakiimba nyimbo.
Usalama umeimarishwa jijini Nairobi huku zaidi ya maafisa elfu kumi wakitumwa katika uwanja huo na maeneo mengine ya Nairobi kuweka usalama.
Siku ya Ijumaa Raila aliwaomba wafuasi wake wadumishe amani wakati wa mkutano wa kumkaribisha katika uwanja wa Uhuru Park jijini humo.
Hayo yakijiri viongozi wakuu wa mrengo wa Cord wamekodisha mabasi kutoka ngome zao kuu kuwasafirisha wafuasi wao hadi Nairobi ili kuhudhuria mkutano huo wa kumkaribisha kiongozi wao.
Katika kaunti ya Mombasa gavana Hassan Ali Joho amesema kuwa mabasi 25 yamewasafirisha wafuasi wa Cord kuhudhuria mkutano huo wa Nairobi.