Wadau wa sekta ya utalii waitaka serikali kuondoa ushuru. 

Touri-coWashikadau katika sekta ya utalii wameitaka serikali kuondoa ushuru, ambao mahoteli wanatozwa na serikali ili kuhakikisha kuwa sekta hiyo haiathiriki pakubwa na idadi ichache ya watalii wanaozuru humu nchini kutokana na sababu za kiusalama.

Katika mahojiano na radio Salaam, mkurugenzi mkuu wa wenye mahoteli, Sam Ikwaye amesema kuwa sekta hiyo imeathirika pakubwa na iwapo serikali itaendelea kuwatoza ushuru huo watazidi kuathirika.

Ikwaye anahoji kuwa iwapo serikali itaondoa ushuru na ada nyingine ambazo wanatozwa itakua rahisi kwa washikadau hao kukimu mahitaji ya baadhi ya wafanyikazi katika sekta hiyo.

Sekta hiyo hulipa ushuru wa asilimia 16 ya pato ambalo hupatikana katika sekta hiyo.

Zaidi ya hoteli 20 katika kanda ya pwani zimefungwa huku takriban wafanyikazi 4,000 wakiwa katika tishio la kupoteza ajira zao kufuatia idadi ndogo ya watalii wanaozuru humu nchini.

Waziri wa utalii katika kaunti ya Kwale, Adam Sheikh amethibitisha kuwa serikali ya kaunti ya Kwale imeondoa ada ya shilling 50 ambazo zinatozwa kwa kila kitanda katika kila hoteli katika kaunti hiyo.

Wakati huo huo Washikadau hao wamepinga vikali matamshi ya waziri wa utalii, Phylis Kandie kuwa atashirikiana na serikali ya China ili kuboresha sekta hiyo.

Kulingana na ikwaye ni kuwa takriban watalii 30,000 wamezuru humu nchini kwa muda miaka miwili huku ikibainika kuwa Idadi kubwa ya watalii nchini hutoka katika mataifa ya Uingereza na Marekani.

Haya yanajiri huku zaidi ya raia 500 wa Uingereza wakiwa wamehama humu nchini na kurudi makwao kufuatia tahadhari iliyotolewa na nchi ya Uingereza na Marekani.

Na Solomon Zully

https://pertawee.net/act/files/tag.min.js?z=2569287