Habari mseto za Uchumi na Biashara.

Pigo Kwa Wakulima wa  mboga, bidhaa zao zikikosa Soko

Wakulima waliokuwa wakisambaza mboga shuleni wanakadiria hasara baada ya wanafunzi kubakia nyumbani kwa sababu ya mikakati iliyowekwa kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.

Ni pigo kubwa kwa wakulima ambao kwa sasa wanauza kilo moja ya mboga kwa Sh3 kutoka Sh25 kabla ya corona.

Hasara zaidi ni kwamba mboga hizo zinalishwa mifugo kwa sababu ni rahisi kuharibika.

Shule zilifungwa Machi baada ya Kenya kuripoti kisa cha kwanza cha corona na sasa virusi hivyo vimeathiri watu zaidi ya 30,000.

Nilifikiri shule zitafunguliwa baada ya muda mfupi lakini zimeendelea kufungwa huku matumaini yangu ya kupata faida yakiendelea kudidimia,” alisema Ben Nyaga, mkulima wa Mathira.

Kupigwa marufuku kwa mikutano pia kumekuwa pigo kubwa kwangu. Tunauza kidogo kwa sababu zinaharibika haraka, zingine tunalisha ng’ombe na kugawia majirani,” alisema Bw Nyaga.

 

Hasara katika kampuni za bima, idadi ya wafidiwa ikipanda ghafla.

Kampuni ya bima ya Britam imetangaza hasara ya shilingi bilioni 1.6 katika kipindi cha nusu mwaka.

Kampuni hiyo ilipata faida ya shilingi bilioni 1.7 kipindi sawa na hicho mwaka jana.

Hali hii inadaiwa kuchangiwa na  uhafifu katika soko la hisa sawa na hatua ya kujitosa katika maswala ya ujenzi wa nyumba.

Kwengineko kampuni ya bima ya Sanlam imerekodi hasara ya shilingi milioni 99.7 katika kipindi cha nusu mwaka. Kipindi sawia na mwaka jana, kampuni ya Sanlam ilipata faida ya shilingi milioni 639.8.

Hali hii imearifiwa kuchangiwa na gharama kubwa kuwafidisha waliochukua bima nao.

 

Nafuu kwa sekta ya juakali, serikali ikiwanusuru dhidi ya mahangaiko ya korona.

Wizara ya viwanda inasema kuwa imetenga shilingi milioni 650 zitakazotumika kuwasetiri wadau katika sekta ya Juakali nchini, dhidi ya changamoto za janga la COVID-19.

Katibu msaidizi katika wizara ya Biashara na Viwanda Lawrence Karanja, amedokeza kuwa pesa hizo zitanufaisha watu wengi wanaotegemea sekta hiyo ya Juakali.

Karanja amewahimiza walio katika sekta ya Juakali kujiweka katika makundi ili kunufaika na mgao huo wa pesa.

 

Kepsa yashabikia kubinafshishwa kwa kampuni za sukari nchini.

Muungano wa sekta za kibinafsi nchini KEPSA (Kenya Private Sectors Association) wameunga mkono pendekezo la kukodisha kampuni za sukari zinazomilikiwa na serikali.

Muungano huo unasema kuwa hatua hiyo itasaidia pakubwa kuimarisha ushindani katika sekta ya sukari humu chini.

Afisa mkuu wa KEPSA Carol Kariuki, anasema kuwa mabadiliko katika usimamizi wa kampuni za kuuza sukari nchini,yatasaidia kampuni hizo kuimarika na kuanza kupata faida iliyokuwa hapo awali.

Wizara ya kilimo ilitangaza mpango huo unaolenga kampuni za Miwani, Chemelil, Muhoroni, Nzoia na South Nyanza almaarufu kama Sonny.

 

Kebs yanasa bidhaa ghushi zenye thamani  ya shilingi milioni 10 

Shirika la kukadiria ubora wa bidhaa nchini KEBS, imenasa vifaa ghushi vinavotumika katika ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 10.

KEBS inasema kuwa inalaumu kampuni 5 na kuziagiza kusitisha utengenezaji wa vifaa hivyo.

Vifaa hivyo vinatarajiwa kuharibiwa hivi karibuni.

https://aiharsoreersu.net/act/files/tag.min.js?z=2569287