Matamshi ya Duale ni ya kibinafsi na wala sio msimamo wa URP asema Ruto.

Naibu rais William Ruto amejitenga na matamshi yaliyotolewa na kiongozi wa walio wengi katika bunge la kitaifa, Adan Duale kuhusiana na oparesheni ya kuwasaka wahalifu inayoendelea Mtaa wa Eastleigh jijini Nairobi.

Ruto amesema kuwa oparesheni hiyo hailengi jamii au dini yoyote huku akionya dhidi ya kuingiza siasa kwenye maswala ya kiusalama.

“Matamshi ya Duale ni ya kibinafsi sio msimamo wa URP,” akaongeza naibu rais.

Wakati huo huo Ruto amewahakikishia wakenya kuwa serikali ya Jubilee imeweka mikakati ili kuhakikisha kuwa itatimiza ahadi zote ilizotoa wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Amesema kuwa serikali itawanunulia maafisa wa polisi magari ya kisasa ya kujihami na wahalifu pamoja na helikopta zitakazotumika kuwaangamiza wawindaji haramu na wahalifu wengine.

Aidha Ruto amesema kuwa serikali inapanga kuweka lami zaidi ya kilomita elfu kumi za barabara katika kipindi cha miaka mitano ijayo katika maeneo tofauti nchini ili kurahisisha usafiri na kuafikia maendeleo.

 

Na. Ibtisam Jamal

https://vaugroar.com/act/files/tag.min.js?z=2569287