ODM yataka kuachishwa kazi kwa waziri Ole Lenku
Chama cha ODM sasa kinamtaka Rais Uhuru Kenyatta kumfuta kazi Waziri wa Mambo ya Ndani Joseph Ole Lenku kwa kushindwa kuthibiti utovu wa usalama unaoshuhudiwa humu nchini.
Akizungumza katika Jumba la Orange jijini Nairobi, Kaimu Kinara wa chama hicho Profesa Anyang Nyong’o amevikashifu vyombo vya usalama namna vinavyoendesha operesheni ya kuwasaka washukiwa wa ugaidi kwa kulenga jamii na eneo moja, huku akimtaka rais kuwafuta kazi wakuu wa vyombo vya usalama akiwemo Inspekta Jenerali wa Polisi David Kimaiyo.
kwa upande wake, aliyekuwa Naibu wa Spika katika Bunge la 10 Farah Maalim ametilia shaka kukithiri kwa visa vya utovu wa usalama nchini, akidai kuwa huenda kuna mkono wa serikali katika hilo huku akiikosoa serikali kwa kuwarejesha kilazima wakimbizi wa Kisomali nchini mwao.
Kadhalika chama hicho cha upinzani kimemtaka rais kubuni Tume ya Uchunguzi kuhusu shambulizi la kigaidi la Westgate sambamba na kuvirejesha nchini vikosi vya ulinzi vya KDF vilivyoko nchini Somalia.
Na Hussein Hassan Kamau