Shirika la Kidogo Early Years kuendelea kuimarisha vituo vya kulelea watoto (Day Care Centres) nchini.
Shirika linaloangazia maslahi ya watoto hasa wanaolelewa katika vituo vya malezi yaani Day Care Centres, la Kidogo Early Years, linaendeleza mikakati ya kuimarisha hali ya vituo hivyo ili kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira yanayostahili.
Mshauri mkuu wa maswala ya ushirikiano katika Shirika hilo Martina Adega amesema kufikia sasa Shirika hilo limesajili jumla ya vituo 1,600 na kuwafikia zaidi ya watoto 38,000 katika maeneo mbalimbali nchini, huku Shirika hilo likiimarisha hali ya vituo hivyo.
Akizungumza Mjini Mombasa hii leo ambako Shirika hilo limefikia zaidi ya watoto 5,000 katika huduma hiyo, Martina amesema kwa sasa Shirika hilo linapania kupanua huduma zake katika Kaunti ya Mombasa ili kuhakikisha vituo vya watoto vinasajiliwa, vinazingatia sheria na vinaendeleza shughuli zake katika mazingira yanayostahili.
Afisa huyo amehoji kwamba jitihada hizo zinalenga kuboresha mazingira ya vituo hivyo na wala sio kwa vituo hivyo kuendeleza harakati zake kiholela na kuwaweka watoto katika hatari.
Kwa upande wake, Afisa mkuu wa maswala ya sera na ushirikiano katika Shirika hilo Elaine Wacuka Hurt amekiri kuwepo na changamoto katika vituo vya malezi vya siku, japo akasisitiza kwamba wanafanya kazi na Serikali ya kitaifa na zile za Kaunti ili kuibuka na sera itakayosawazisha hali katika vituo hivyo.