Benfica FC Mabingwa Ali Mbogo Super Cup,Mbogo akiahidi makubwa.

Timu ya Benfica FC ndio Mabingwa wa michuano ya Ali Mbogo Super Cup 2023 baada ya kuilaza Ajax FC mabao 2-1 katika mechi ya fainali iliyochezwa uga wa Kadongo eneo bunge la Kisauni.

Benfica wametuzwa kititta cha shilingi laki moja na elfu hamsini pamoja na kikombe huku timu ya Ajax FC ikituzwa shilingi elfu 75. Awali kila timu ambayo ilishiriki mashindano hayo ilikabidhiwa seti moja ya jezi pamoja na mipira miwili.

Michuano hiyo ilidhaminiwa na mwenyekiti wa mradi wa LAPSET na aliyekuwa mbunge wa eneo hilo la Kisauni, Ali Mbogo.

Akiongea na waandishi wa habari mdhamini huyo Mbogo amesema lengo la kuwaleta wanajamii pamoja na kuishi kwa Amani licha ya tofauti za kisiasa zilizokuwa zikishuhudiwa zimetimia kupitia michuano hiyo na kuahidi kupanua zaidi michuano ya makala yajayo.

Mbogo amesema pia anapania kukuza vipaji vya mziki kupitia Talanta Show katika kipindi hiki cha likizo kubwa ili kuwaepusha vijana kujiunga na kushiriki katika makundi ya uhalifu pamoja na kutumia mihadarati.

 

 

Aidha Mbogo amesema michuano hiyo imefungua nafasi kwa vijana kwenda kusakata kandanda nje ya nchi.

Mbogo akiahidi kushirikiana na viongozi walioko madarakani katika kaunti ya Mombasa ili kulinda na kuboresha hadhi ya viwanja vya mpira katika eneo bunge la Kisauni.

 

Kwa upande wake mkufunzi wa mabingwa wa michuano hiyo Benfica FC Mohammed Bachu amemshukuru mdhamini wa michuano hiyo Ali Mbogo kwa kuanzisha michuano hiyo akisema ni njia moja ya kutambua na kukuza talanta huku akiwamwagia sifa wachezaji wake kwa kuwa na heshima na kujituma mchezoni jambo ambalo limechangi wao kuibuka mabingwa.

Bachu aliongezea kusema kwamba pesa walizotuzwa watazitumia kwa manufaa ya timu na wachezaji wake.