Wanafunzi Mombasa wafaidika na mradi wa sodo wa Seneta Miraj Abdillah.
Huenda tatizo la wanafunzi wa kike katika shule za msingi na sekondari kukosa kuhudhuria shule kwa kukosa kutumia sodo wakati wa siku zao za hedhi likamalizika katika ukanda wa pwani,hii ni baada ya juhudi za seneta maalum Miraj Abdillahi la kumaliza swala hili kushuhudiwa kila uchao.
Akiongea katika hafla ya kusambaza sodo kwa wanafunzi katika shule ya msingi ya Central Girls hapa Mombasa,Miraj amesema ni jukumu lao kama viongozi kuona kwamba wanawajibika na kila mwanafunzi wa kike hakosi kuhudhuria shule kwa kukosa kutumia sodo.
Miraj amesema vitendo vya wanafunzi hao kukosa shule kwa Zaidi ya siku kumi katika muhula kunawarudisha nyuma kimasomo na kuchangia kutofanya vyema katika mitihani yao.
Aidha Miraj amewataka wanafunzi hao kutambua haki yao ya elimu na kutia bidii katika masomo ili kuweza kufaulu katika maisha yao na kuisaidia jamii.
Miraj amesema atashirikiana na washikadau mbalimbali wa elimu kuhakikisha mtoto wa kike amewezeshwa ili kuweza kufaulu na kutimiza ndoto zake maishani.
Kadhalika Miraj amesema ukosefu wa sodo kwa wanafunzi wa kike haufai kutumika kama kigezo cha kuwakandamiza kielimu.
Miraj amesikitishwa na hatua ya serikali ya kupeana mipira ya kondomu bure kwa jamii ilhali kuna wanafunzi wa kike ambao wanakosa shule kwa kukosa kutumia sodo jambo ambalo mara kadhaa hufanya wanafunzi hao kurubuniwa na sodo na kufanyiwa vitendo vya kinyama.
Pia amesema kuna haja ya maseneta wenzake kupitisha mradi wake wa kumlinda motto wa kike ili kutoa fursa nyengine ya elimu kwa wote waliopachikwa mimba na kutelekeza masomo.