Ali Mbogo Super Cup kutimua kivumbi Kisauni.
Michuano ya soka ya Ali Mbogo Super Cup kungoa nanga rasmi mnamo tarehe 9 mwezi wa septemba huku mshindi wa michuano hiyo akitarajiwa kutunukiwa pesa taslim ksh. 150,000 nae mshindi wa pili kutia kibindoni shilingi 75,000.
Michuano hiyo ambayo yanadhaminiwa na mwenyekiti wa mradi wa LAPSET na aliyewahi kuwa mbunge wa Kisauni Ali Mbogo,imevutia timu 16 kutoka wadi tatu za Junda,Magogoni na Mjambere na kugawanywa katika makundi manne ambapo kila kundi limebeba timu nne.
Kundi A linajumuisha PSG, B13 FC, Cameroon FC na Bilima Youth FC nalo Kundi B linakutanisha Team 27 FC, Junda Strikers FC, Real Juniors FC na Coast United FC wakati Kundi C lina Benfica, GoodHope FC, Junda United FC na Wazito FC. Nazo timu za Ajax, Black Stars FC, Vestax FC na Kangumuu FC zimepangwa kwenye Kundi la mwisho la D.
Mashindano hayo yatafunguliwa rasmi tarehe 9 septemba huku mechi ya ufunguzi ikiwa kati ya PSG dhidi ya B13 FC,ambapo wata garagizana katika uwanja wa Kadongo katika eneo bunge la Kisauni.
Kila timu inayoshiriki mashindano hayo itazawadiwa seti ya jezi na mipira miwili. Michuano hiyo inatarajiwa kukamilika siku ya Ijumaa Oktoba 20,2023 kwa mechi ya lala salama ya mashindano hayo ya fainali ambapo bingwa atajulikana na kutuzwa.