Wanawake 40 pwani kunufaika na mafunzo ya uchumi wa baharini.
JUMLA ya wanawake 40 kutoka Kanda ya pwani wanalengwa kuwezeshwa kupitia mpango wa elimu ili kunufaika na uchumi wa rasilimali za bahari unaotekelezwa na mashirika na kampuni mbalimbali ikiwemo kampuni ya ushauri ya Basket One.
Chini ya mpango huo maafisa maalum watatwikwa jukumu la kuwaelimisha wanawake hao ili kuafikia malengo endelevu yanayokusudiwa kwenye mradi huo.
Akiongea na waandishi wa habari katika kaunti ya Mombasa mwakilishi wa kampuni ya ushauri ya Basket One James Wekesa ,amesema watachagua wanawake 40 kutoka kaunti sita za pwani ambao watafaidika na elimu hiyo na kupitia mafunzo ambayo yatatolewa na wakufunzi maalum, hii ni baada ya kugundua wanawake wengi hawana ufahamu kuhusu uchumi samawati.
Aidha amedokeza kuwa miongoni mwa mafunzo wanayonuia kuwaelimisha ni mbinu bora za ufugaji wa Samaki, kuboresha mavuno ya mwani pamoja na mafunzo mengine yanayohusu uchumi wa shughuli za baharini.
Wekesa amesema wataweka mikakati maalum ya kupambana na changamoto ambazo kina mama hao wanapitia ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa urahisi.
Kwa upande wake Agnes Machache mmoja wa akina mama anayelengwa kunufaika na mradi huo amesema fursa hiyo itamuwezesha pakubwa kutatua baadhi ya changamoto zinazomkabili kama mvuvi wa kike.
Uzinduzi rasmi wa shughuli hyo itafanyika tarehe tarehe tano mwezi huu siku ya Jumamosi.