EACC yazitaka bodi za wataalamu kuwa mstari mbele katika vita dhidi ya ufisadi
TUME ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC imezitaka bodi za wataalamu kuunga mkono agenda ya kitaifa ya kukabiliana na ufisadi kwa kushinikiza maadili mema miongoni mwa wanachama wao ili kukabiliana na tatizo la ufujaji wa fedha serikalini.
Tume hiyo imesema kuwa wakenya wanawatarajia wataalam serikalini kutumia elimu na maarifa waliyonayo kwa ajili ya kuleta maendeleo kwenye jamii na wala si kufanikisha vitendo vya ufisadi au kushiriki mipango ya kuwadhuru.
Akihutubia wanahabari kwenye kaunti ya Mombasa wakati wa kufunga warsha ya wiki moja iliyowaleta pamoja maafisa watoa zabuni katika serikali ya kitaifa na zile za kaunti kote nchini ,Msemaji wa tume ya EACC Eric Ngumbi amebainisha kuwa licha ya sheria kubuni bodi za wataalamu ili kuongoza taaluma mbalimbali , ni mafanio machache tu yaliyopigwa katika kujenga maadili mema miongoni mwa wanachama kwenye bodi hizo.
kutokana na hilo Ngumbi amedai kuwa bodi nyingi za wataalamu bado hazijatekekeza jukumu lao kikamilifu kama mawakala wa kushinikiza uongozi bora.
Amedokeza kuwa uchunguzi uliyofanywa na tume ya EACC umebainisha kuwa hakuna kashfa yoyote ya kubwa ya ufisadi iliyotekelezwa nchini bila ya kuhusishwa kwa mtaalamu, hivyo ameshinikiza haja ya ushirikiano baina ya tume ya EACC na bodi hizo kwa nia ya kuwajenga wafanyikazi kuwa na maadili mema zaidi.
Na Kama njia moja wapo ya kukabiliana na tatizo la ufisadi nchini Ngumbi amevirai vyuo vikuu nchini kuanzisha kozi maalumu ya kufunza maadili mema miongoni mwa wanafunzi ili kuwawezesha kuwa raia wema pindi watakapopata ajira katika taaluma mbalimbali walizosomea.