Seneta Miraj aukosoa upinzani kwa kupinga mapendekezo ya mswada wa fedha wa mwaka 2023

SENETA maalum wa kaunti ya Mombasa kupitia chama cha UDA Miraj Abdillah kwa mara nyengine amewakosoa wanasiasa wa upinzani nchini kwa kuendelea kupinga pendekezo la kuwatoza wafanyikazi asilimia tatu ya mishahara yao ili kuchangia kwenye mradi wa serikali ya kitaifa wa hazina ya nyumba.
Kulingana na Miraj ni kinaya kuona wanasiasa hao wakiwa mstari mbele kupinga pendekezo hilo lilojumuishwa kwenye mswada wa fedha wa mwaka 2023 ilhali hawajatoa suluhu mbadala kutatua tatizo la ukosefu wa makaazi ya kutosha nchini.
Ameyazungumza hayo wakati akihutubia kwenye hafla ya uzinduzi wa kundi la vijana la The Amplified youth, ambapo amewataka wanasiasa wa mrengo wa upinzani kusitisha kile alichokitaja kutokuwa na nia njema katika mjadala unaohusu mswada wa fedha wa mwaka 2023, badala yake amewarai waunge mkono agenda za serikali ya kitaifa ili kuleta maendeleo kwa wakenya.

Wakati huo huo ameeleza kuwa serikali ya Kenya Kwanza chini ya rais William Samoei Ruto tayari imeweka mipango madhubuti ya kuhakikisha ahadi zote walizozitoa kwa wakenya wakati wa kampeni zinatimizwa.
Kwa upande wake mbunge wa Kenya kwenye bunge la Afrika Mashariki ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa Chama cha UDA Hassan Omar Sarai amewatahdhrisha wakaazi wa kaunti ya Mombasa dhidi ya kutumiwa visivyo na wanasiasa kwa maslahi yao binafsi.

Sarai amesema inasikitisha kuona kwa miaka mingi wakaazi wa kaunti hiyo wamekuwa wakihadaiwa na wanasiasa jambo linalosabisha waendelee kusalia nyuma kimaendeleo.
Aidha ameshinikiza haja ya ushirikiano wa pamoja baina ya wanasiasa wote kaunti ya Mombasa kwa kutojali misingi ya chama ili kuhakikisha kuwa wakaazi wananufaika na miradi ya serikali.
Vile vile Sarai amewarai wabunge wa chama cha ODM kwenye kaunti hiyo kuungana wenzao wa Kenya Kwanza ili kuupitisha mswada wa fedha wa mwaka 2023 ambao tayari uliyowasilishwa kwenye bunge la kitaifa.
Wakati wa hafla hiyo Sarai alitoa kitita cha shiligi milioni 3.7 kama mtaji kwa kundi la vijana la The Amplified youth ili kuwawezesha kuanzisha miradi ya biashara na kujikwamua kiuchumi.

Vijana wa kundi hilo wakiongozwa na Martha Asena wamemshukuru sarai kwa kubuni mpango wa kupiga jeki makundi ya akina mama na vijana kwenye hiyo huku wakiahidi kuunga mkono kikamilifu agenda za serikali ya Kenya Kwanza.