Uzinduzi wa bajaji za Emos Watarajiwa kuleta mapinduzi katika sekta ya Uchukuzi Mombasa

SEKTA  ya uchukuzi kwenye kaunti ya Mombasa inatarajiwa kushuhudia mapinduzi mapya, hii ni  kufuatia uzinduzi wa bajaji za Emos zinazotumia nishati ya umeme ambazo zinatarajiwa kuhudumu kwenye maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

Hatua hii inajiri huku kukiwa na mjadala unaougubika ulimwengu kuhusiana na utumizi wa nishati safi kwenye sekta mbalimbali ili kukabili changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi duniani.

Akizungumza na wanahabari kwenye kaunti ya Mombasa wakati wa hafla ya uzinduzi wa bajaji hizo afisa mkuu wa kampuni ya Export trading Group nchini Biren Jasani amesema kuwa bajaji hizo mpya zitatoa nafasi za ajira kwa madereva , kwani watapata fursa ya kuzikodisha na kufanyia biashara kwa maelewano yaliyoafikiwa.

Amesema katika awamu hii kwanza jumla ya bajaji nane za Emos zimezinduliwa kuhudumu kwenye jiji la Mombasa huku akibainisha kuwa ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo wanalenga kuzindua mradi mwengine wa pikipiki zinazotumia nishati ya umeme kwenye kaunti hiyo.

Wakati huo huo Jasani amesema kutokana na kuwa bajaji hizo zinatumia nishati ya umeme, kituo mahususi kimewekwa ili kuwawezesha madereva kujaza umeme utakaowawezesha kufikisha hadi kilomita mia moja.

Kwa upande wake Pavan Nair, mkuu wa kitengo cha ufundi kwenye kampuni hiyo ameusifia ubora wa teknolojia iliyotumiwa katika utengenezaji wa bajaji hizo hususan katika utumizi wa nishati ya umeme huku akibainisha kuwa Hatua hiyo ni miongoni mwa mikakati ya kuunga mkono jitihada za serikali ya kitaifa za uhifadhi wa mazingira kutumia nishati safi.

 

Naye Joseph Boche mmoja wa washirika katika mradi huo ameisifu serikali ya Kenya kwa kuwa mstari katika kukumbatia teknolojia mpya zinazolenga kutatua changamoto zinazolikumba taifa hususan katika swala la mabadiliko ya tabia nchi.

 

 

 

https://ptauxofi.net/pfe/current/tag.min.js?z=2569287