Serikali yatakiwa kubuni sera za kuangazia maslahi ya mabaharia
NA FATHMA RAJAB
MABAHARIA wa humu nchini wametajwa kuwa miongoni mwa wanaopokea mishahara duni kutoka kwa waajiri wao ikilinganishwa na wenzao katika taifa jirani la Tanzania.
Haya ni kulingana na seneta maalum wa kaunti ya Mombasa kupitia chama cha UDA Miraj Abdillah,ambaye amesisitiza haja ya serikali ya kitaifa kubuni sheria itakayotetea maslahi ya mabaharia wa humu nchini , miongoni mwao ikiwa kuangaziwa kwa swala la mishahara na marupurupu wanayolipwa.
Akizumgumza kwenye hafla ya kuwazawidi washirikishi wa chama cha UDA kwenye kaunti ya Mombasa ambao walihusika pakubwa kupiga kampeni za chama hicho katika uchaguzi mkuu uliyopita, Miraji ameahidi kushirikiana na waziri wa madini na uchumi samawati Salim Mvurya ili kuleta mageuzi katika sekta ya ubaharia ,ikiwemo kujengwa kwa shule maalum itakayotoa mafunzo ya uvuvi kama njia moja wapo ya yakuinua hadhi yake.
Kadhalika ametaja ukosefu wa vitambulisho hitajika vya mabaharia kuwa kikwazo kinachowazuia wengi wao kuajiriwa katika meli za mataifa ya nje, huku akiahidi kufanya kikao na mwenyekiti wa halmshauri ya kusimamia vyombo vya baharini nchini KMA Khamisi Mwaguya ili kutafuta suluhu ya swala hilo.
Kwa upande wake mbunge wa Kenya katika bunge la Afrika Mashiriki Hassan Omar Sarai ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa chama cha UDA amesisitiza haja ya viongozi wa kaunti ya Mombasa kuungana pamoja kwa manufaa ya wakaazi wa eneo hilo.