Mabadiliko ya tabia nchi yatajwa kuathiri mifumo ya afya nchini

WADAU  katika sekta ya afya wanaohudhuria Kongamano la 50 la sayansi linaloandaliwa na muungano wa madaktari nchini KMA kwenye kaunti ya Mombasa, wametaja changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi kuathiri pakubwa mifumo ya afya hapa nchini  na bara la Afrika kwa ujumla.

Wadau hao vile vile wamepigia upatu matumizi ya teknolojia na uvumbuzi katika kusuluhisha changamoto zinazotokana na mabadiliko hayo.

Hatahivyo akihutubia wanahabari wakati wa hafla ya ufunguzi rasmi wa kongamano hilo rais wa muungano wa madaktari nchini KMA  Simon Kingondu amedokeza kuwa ili kukabiliana kikamilifu na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi, serikali ya kitaifa inapaswa kuboresha mfumo mzima wa afya kwa kujenga vituo zaidi vya afya sawia na kuongeza idadi madaktari na wafanyikazi wengine watakaohudumu kwenye vituo hivyo.

Kadhalika Simon amedokeza kuwa Kongamano la Mwaka huu linawiana na  maadhimisho wa miaka 100 tangu kuasisiwa kwa jarida la afya la Afrika Mashariki ambalo limekuwa muhimili mkuu wa kuchapisha  miongozo mbalimbali na tafiti za kisayansi  zinazohusu sekta ya afya.

Kwa upande wake gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya ufunguzi wa kongamano hilo, amebainisha kuwa serikali yake inanuia  kuzindua  mpango wa Afya care ambao kufikia Mwezi Disemba mwaka huu,  jumla ya familia 15,000  kwenye kaunti hiyo zitakuwa zimenufaika na bima ya afya.

Wakati huo huo  Nassir amedokeza kuwa tayari serikali yake imeajiri madaktari zaidi katika hospitali za umma  ili kuimarisha jitihada za kukabiliana na virusi vya Rota Virus ambavyo viliripotiwa kuzuka awali kwenye kaunti hiyo.

Nao maafisa wanaohudhuria kongamano hilo kutoka wizara ya mazingira kitengo cha  kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, wamesisitiza kujitolea kwa serikali ya kitaifa katika kutimiza ajenda yake ya upanzi wa miti bilioni kumi 15 ndani ya kipindi cha miaka kumi ijayo ili kudhibiti zaidi athari ya mabadiliko ya tabia nchi nchini.

Aidha wamesema kuwa kama wizara wanasimamia utekelezwaji wa sheria ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira ya mwaka 2010 ili na kufanikisha uchakatishaji wa taka zinazotupwa kiholela kuwa bidhaa zinazoweza kutumika katika mahitaji mengine kuhifadhi mazingira.

https://ptauxofi.net/pfe/current/tag.min.js?z=2569287