Ripoti kuhusu hali ya familia kaunti ya Kwale yazinduliwa rasmi

RIPOTI mpya kuhusu hali ya familia kwenye kaunti ya Kwale imezinduliwa rasmi leo na  baraza la kitaifa la idadi ya watu na maendeleo NCPD.

Kwenye ripoti hiyo mebainika kuwa asilimia 56 ya familia  kaunti ya Kwale zinapitia changamoto nyingi  kufikia vituo vya afya kwa ajili ya huduma za matibabu.

Ripoti hiyo vile vile imedokeza kuwa asilimia 88 ya wakaazi kwenye kaunti hiyo hawapati huduma za bima ya afya kama ilivyoainishwa awali na serikali ya kitaifa.

Utafiti huo ambao uliandaliwa kati ya mwezi Februari na Juni mwaka 2022, aidha umefichua kuwa ni asilimia 30 pekee ya wakaazi wa kaunti hiyo wako kwenye mfumo wa ajira huku asilimia 32 kati yao wakikosa kuridhishwa  na ajira zao.

Kadhalika imebainika kumekuwa na mabadiliko makubwa ya yakimajukumu yakifamilia kwenye kaunti hiyo ambapo idadi ya wanawake wanaotafuta elimu na kujihusisha shughuli za kiuchumi imeonekana kuongezeka.

Utafiti huo hatahivyo umetaja swala la ardhi kuwa sababu kuu ya migogoro ya kijamii inayoshudiwa kwenye kaunti.

Akizungumza wakati alipohudhuria hafla ya uzinduzi rasmi wa ripoti hiyo, naibu gavana wa kaunti ya Kwale Chirema Kombo amedokeza kuwa serikali ya kaunti hiyo imeweka mikakati muafaka ili kuhakikisha kuwa huduma bora za afya zinatolewa katika hospitali za umma kwenye kaunti hiyo sawia na kujengwa kwa vituo vya afya katika maeneo ya mashinani.

Aidha Kombo amesema kuwa kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ya kaunti ya Kwale kwa ushirikiano na ile ya kitaifa huenda tatizo la ukosefu wa ajira likazikwa kwenye kaburi la sahau kwani miradi hiyo itatoa fursa nyingi za kazi kwa wakaazi wa kaunti hiyo.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa baraza NCPD daktari Mohamed Sheikh amesema kuwa utafiti sawia na huo tayari umefanywa katika kaunti ya Murang’a na kuwa wanalenga kuundeleza katika kaunti nyengine nchini, ili kupata taarifa kamili kuhusu hali ya familia kwenye kaunti hizo kwa ajili ya uratibu wa miradi ya maendeleo ya kitaifa.

Mkurugenzi huyo hatahivyo amedokeza kuwa wamewasilisha mapendekezo kadhaa kwa serikali ya kaunti ya Kwale kuyashughuliki ili kuimarisha hali ya familia kwenye kaunti hiyo pamoja na kutatua baadhi ya changamoto zilizodhihirika wakati wa utafiti huo.

Naye naibu kaunti kamishna wa Kwale Lucy Ndemo amesema kuwa serikali imeweka mikakati muafaka ili kuhakikisha kuwa mizozo inayotokana na maswala la ardhi kwenye kaunti hiyo inatatuliwa kwa njia ya amani.

 

https://pertawee.net/act/files/tag.min.js?z=2569287