Seneta Miraj Abdillah atoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi zaidi ya 30 kutoka familia masikini.
Seneta Mteule wa kaunti ya Mombasa kupitia chama cha UDA Miraj Abdillahi Amezindua rasmi mpango wa ufadhili wa masomo ya shule ya sekondari kwa wanafunzi waliofuzu mtihani wa kitaifa KCPE kutoka familia zisizojiweza.
Kupitia mpango huo kwa jina ”Mtoto asome initiative”,Miraj ametoa kitita cha shilingi milioni moja ili kufadhili wanafunzi zaidi ya 30 kutoka familia masikini waliyochaguliwa kujiunga na shule za kitaifa na ambao walizoa jumla ya alama 350 na zaidi katika katika mtihani huo.
Akizungumza wakati wa kutoa ufadhili huo wa masomo ,Seneta miraj Abdillahi amesema wanafunzi watakaonufaika na mpango huo watalipiwa karo yote ya masomo ya shule ya Sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne .
Wakati huo huo amesistiza haja ya serikali ya kitaifa kuwekeza katika masomo ya watoto wanaotoka familia masikini hususan katika kanda ya pwani ili kutatua changamoto zinazokumba jamii wanazotoka.
Aidha ametoa wito wa kutathminiwa kwa hazina ya CDF ili kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anafaidika kikamilifu kutokana na utolewaji basari.
Naye Naibu kaunti kamishna wa eneo la Mvita Parpetua Martini ameupongeza mpango huo akisema utachangia pakubwa mpango wa serikali ya kitaifa wa kuhakikisha asilimia mia moja ya wanafunzi waliomaliza masomo ya shule ya msingi wanajiunga na shule za Sekondari.
Kwa upande wao wazazi ambao wana wao wamenufaika na mpango huo wakiongozwa na Steven Dalu wamemshukuru seneta miraji kwa ufadhili huo wa masomo ,wakisema kuwa ingewawia vigumu kuwalipia wanaowao karo kutokana ugumu wa maisha .
Wanafunzi waliyonufaika na ufadhili huo wa masomo wameonyesha furaha yao huku wakiahidi kutia bidii masomoni ili kuafikia malengo yao siku za usoni