Wanawake Supkem wampongeza Nassir kwa uteuzi wa baraza la mawaziri

Mtandao wa wanawake wa Baraza kuu la Waislamu hapa nchini Supkem tawi la Mombasa umempongeza gavana wa kaunti hiyo Abdulswamad Shariff Nassir kwa kuwateua wanawake wawili wa dini ya kiislamu katika baraza lake la mawaziri Sawia na kuzingatia umuhimu wa mashirika ya kijamii katika baraza hilo.
Wakiongozwa na Riziki juma Wanawake wa mtandao huo kutoka maeneo bunge yote sita ya kaunti ya Mombasa, wameutaja uteuzi wa Kibibi Khamisi Abdalla na Swabaha Ahmed Omar kuwa mwanzo mpya wa kutambua uongozi wa wanawake hususan wa dini ya kiislamu katika nyadhfa mbalimbali serikalini.
Aidha amesema kuwa uteuzi wa mawaziri hao wanawake utachangia pakubwa kuwachochea wanafunzi wa jinsia ya kike kaunti ya Mombasa kutia bidii masomo ili kufikia ndoto zao siku za usoni.
Kwa upande wake Mshirikishi wa Baraza la Supkem hapa katika kanda ya pwani ya Sheikh Hamisi Juma Mwaguzo Umeutaja uteuzi huo wa baraza la mawaziri kuwa uliyozingia kikamilifu swala la jinsia huku akimtaka gavana Nassir kuendeleza mkondo huo huo kwa kuwateua wanawake zaidi wa dini ya kiislamu kuwa maafisa wakuu katika idara mbalimbali za serikali ya kaunti ya Mombasa.
Wakati huo huo amewahimiza wananchi wa kaunti ya Mombasa kukomesha chuki kwa misingi mbalimbali katika akiwataka wananchi ambao hawajaridhishwa na uteuzi wa baraza hilo la mawaziri kuchukua mkondo wa kisheria kama ilivyoinishwa na katiba.