Ukame watajwa kuongeza visa vya dhulma za kijinsia Marsabit

NA FATHMA RAJAB

VISA vya dhulma za kijinsia vimeripotiwa kuongezeka Katika Kaunti ya Marsabit  huku mamia ya wafugaji wakiendelea kuathirika kutokana na  makali ya ukame unaoendelea kushuhudiwa Katika baadhi ya maeneo nchini.

Makali ya kiangazi yameendelea kuwa changamoto kuu katika familia nyingi za wafugaji Katika Kaunti hiyo  na kuchangia mizozo ya kifamilia kuongezeka zaidi.

Hali hiyo imetajwa kusababisha  ongezeko la matukio ya dhulma za kijinsia majumbani kwani wanandoa wengi hawana uwezo wa kuzikimu familia zao kwa wakati huu.

Kulingana na mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Mwando Nurria Golloh,visa vya dhulma za kujinsia vimeongezeka kutokana na matatizo ya afya ya kiakili kwa wafugaji waliowapoteza mifugo yao kutokana na makali ya ukame wa muda mrefu unaoshuhudiwa Katika Kaunti ya Marsabit.

Aidha  Nurria Pamoja na wadau wengine, wameanzisha harakati za kuwafikia wafugaji kwa kuwapa ushauri nasaha kama sehemu ya kupunguza visa hivyo ambavyo vimeendelea kuongezeka Katika Kaunti hiyo.

Kulingana na afisa mkuu mtendaji wa shirika la kijamii la CIFA Salad Liban ameeleza kwamba,nyingi za visa vya dhulma za kijinsia vimekosa kuripotiwa katika idara ya polisi akifafanua kuwa,wafugaji wengi hawapendi maswala ya kuelekea mahakamani kutafuta haki.

Afisa huyo amehusisha ongezeko la dhulma za kijinsia na ufukara uliosababishwa na kiangazi kilichowauwa mifugo hapa Marsabit.

Marsabit ni miongoni mwa Kaunti  ishirini na tatu yailiyoorodheshwa kuwa katika hali mbaya ya ukame wakati huu.