Shirika la Haki Yetu lazindua ripoti ya makaazi Kaunti ya Mombasa
NA FATHMA RAJAB
Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la utetezi wa Haki kibinaadamu la Haki Yetu kuhusu Hali ya makaazi katika Kaunti ya Mombasa, imebainisha kuwa Serikali ya kaunti hiyo iliyoondoka mamlakani ilishindwa kutekeleza maagizo muhimu iliyopewa na kamati ya seneti kuhusu barabara na uchukuzi Kwa manufaa ya wakaazi wa zamani wa Buxton.
Ripoti hiyo iliyopewa jina Housing for Who imeonyesha kuwa Serikali hiyo ya kaunti ilikuwa ikitoa maelezo yanayokanganya kuhusiana na ardhi ya Buxton yaliyodhamiria kuposha umma kutofahamu ukweli kuhusiana ardhi hiyo.
Akizungumza Kaunti ya Mombasa wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo afisa wa maswala ya ardhi katika Shirika la Haki Yetu Munira Ali amesema kuwa mpango wa kuwaondoa wakaazi hao haukutekelezwa Kwa Kufuata sheria Kwani haukuwa umebainisha mbinu muafaka za kuwaregesha tena baada ya kukamilika Kwa ujenzi wa nyumba za kisasa katika eneo Hilo.
Hatahivyo Munira amesisitiza kuwa ili kukabiliana na swala la makaazi katika Kaunti ya Mombasa Ipo haja ya Serikali mpya ya kaunti hiyo kuangazia kikamilifu swala la ardhi.
kauli yake imeungwa Mkono na John Paul Obonyo afisa kutoka Shirika hilo ambaye ameirai tume ya kitaifa ya ardhi Nchini NLC kuharakisha mchakato wa kusuluhisha visa vya dhulma ya kihistoria za ardhi katika Kaunti hiyo.
Naye mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Gabriel Dolan ametoa wito Kwa Serikali mpya ya kaunti ya Mombasa kuhakikisha kuwa inafanikisha mpango wa makaazi ya bei nafuu Kwa wakaazi wa Kaunti hiyo kikamilifu, Huku akiitahadharisha dhidi ya kushawishiwa Kwa vyote vyote vile na Viongozi wa zamani wa Kaunti hiyo Kwa ajili ya manufaa Yao binafsi.
Kwa upande wake naibu Gavana Wa Kaunti ya Mombasa Francis Thoya amezitaka taasisi husika kushirikiana Kwa pamoja ili kutatua swala ardhi katika Kaunti ya Mombasa akisema kuwa swala la makaazi kwenye Kaunti hiyo litapata ufumbuzi endapo wakaazi watapewa fursa ya kumiliki ardhi zao wenyewe.