Achani amtaka rais Ruto kuwapa nyadhfa serikalini wendani wake wa kanda ya pwani

Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani amemrai Rais William Ruto kuwazawidi nafasi za uwaziri viongozi wa kanda pwani waliyosimama naye na kuhakikisha kuwa anapata kura nyingi katika eneo hilo.
Gavana huyo mpya wa Kwale amemtaja mtangulizi wake Salim Mvurya ,aliyekuwa mbunge wa Malindi Aisha Jumwa,aliyekuwa mbunge wa Kinango Benjamin Tayari pamoja aliyekuwa mbunge wa Msambweni Khatib Mwashetani kama viongozi wanaostahili kupewa nyadhfa za kitaifa katika serikali mpya itakayoundwa, kutokanana na mchango wao wa kumuimarisha rais Ruto kisiasa katika kanda ya pwani.
Aidha Achani amemshukuru rais William Ruto kwa kutimiza ahadi ya kumpa wadhfa wa uspika katika bunge la seneti aliyekuwa gavana wa kaunti ya Kilifi Amason Kingi, akionyesha matumaini kuwa serikali ya Kenya Kwanza itatoa nyadhfa zaidi serikalini kwa wapwani.
Mbali na hayo Achani amedokeza kuwa ukosefu wa dawa katika hospitali za kaunti hiyo umesababishwa na kuchelewa kwa mamlaka ya Kemsa kusambaza dawa katika hospitali .
Wakati huo huo Achani amedokeza kuwa utawala wake utaharakisha mchakato wa ununuzi wa dawa na vifaa vya matibabu ili kuhakikisha kuwa wananchi wa kaunti wanapata huduma za matibabu ipasavyo huku akitoa onyo kwa wahudumu wa afya wanaozembea kazini kuwa watachukuliwa hatua.