Shallo aelekea mahakamani kupinga ushindi wa Machele

Aliyekuwa mgombeaji wa kiti cha Ubunge katika eneo la Mvita kupitia chama cha UDA Omar Shallo ameelekea mahakamani kupinga kuchaguliwa kwa Mohamed Machele kuwa Mbunge wa eneo hilo .
Kupitia kwa stakabadhi alizowasilishwa mahakamani, Shallo anadai kuwa uchaguzi wa Agosti tarehe tisa ambao ulimpa ushindi Machele aliyegombea na chama cha ODM, uligubikwa na kasoro nyingi ikiwemo visa vya kuhonga wakipiga kura ili kumchagua.
Aidha anadai kuwa licha ya baadhi ya vituo vya kupigia kura kufunguliwa kuchelewa, tume ya kusimamia uchaguzi IEBC haikufidia mda uliyopotea wakati wa zoezi hilo, jambo ambalo anasema kuwa liliwakanganya wapiga kura wengi waliyojitokeza kushiriki zoezi hilo.
Wakati huo huo mlalamishi anadai kuwa uchaguzi huo haukuwa wa huru na haki kwani vituo vingi vya kupigia kura ambavyo vilikuwa katika ngome zake za kisiasa vilikumbwa na ghasia zilizoelekezwa kwa mawakala ,wasimamizi wa uchaguzi pamoja na maafisa wa usalama ili kutatiza zoezi hilo kwa makusudi.
Itakumbukwa kuwa machele alitangazwa mshindi na IEBC katika kinyang’anyiro hicho baada ya kuibuka na kura 22,611 huku akifuatwa na Shallo aliyepata kura 11,125.