Timu ya Kishada FC, Mabingwa wa Gago Super Cup

Abdalla Roro wa Longombas FC akipiga mpira kichwa mbele ya Alex Wanjiku wa Kishada
Timu kongwe ya Kishada FC iliizidi nguvu timu ya Longombas kwa kuwalaza bao 1-0 na kunyakua ubingwa wa Kombe la Hassan Gago, uwanjani Bilima bunge la Kisauni.

Bao hilo la kipekee lilitiwa kimiani na mshambuliaji mahiri Allan Masha katika dakika ya 1 ya mchezo baaada ya patashika na uzembe wa mabeki na mlindalango wa Longombas.
Hata hivyo Kishada Fc walilazimika kustahamili makali ya mashambulizi ya Longombas yaliyoongozwa na straika wa zamani wa Bandari na Sony Sugar Joshua Oyoo, katika muda wa dakika zote 90.

Kufuatia ushindi huo Kishada FC walitia kibindoni pesa taslim shilingi elfu 30, Kombe, jezi na zawadi nyinginezo huku mshindi wa wa pili timu ya Longombas ikipewa pesa taslim shilingi elfu 20, kikombe na zawadi.
Kocha wa Kishada Athuman Mwinyishee ameeleza kuridhishwa na matokeo ya vijana wake akipongeza mazoezi yao kwa ushirikiano na uzoefu wao, sawia kudumu pamoja kikosini licha ya changamoto tele ikiwemo changamoto za kifedha.
Mwinyishee ambaye pia aliibuka Mkufunzi bora wa michuano hiyo amepongeza udhamini wa kipute hicho akisema kwamba kutainua motisha wa vijana na kuwasaidia kujimudu na kujiendeleza.

Michuano hiyo iliyoandaliwa uwanjani Bilima, eneobunge la Kisauni ilishirikisha timu 12 kutoka wadi ya Magogoni, huku kila timu iliyoshiriki ikijingakulia jezi na mpira.
Mshindi wa tatu klabu ya Swansea fc ilizawidiwa shilingi elfu 10 pesa taslim na zawadi nyinginezo.
SOMA PIA: https://salaamfm.co.ke/?p=18772&
Mdhamini wa kipute hicho ambaye ni Mgombea Uwakilishi Wadi Magogoni Hassan Mohammed maarufu Gago amesema kuwa Lengo kuu la michuano hiyo ni kuwahamasisha vijana kuzingatia amani na kuepuka vurugu.
Gago alibainisha kuwa ukuzaji talanta na sanaa ni muhimu kwa kuwawezesha vijana kujiendeleza sawia na kuwavua katika utumizi wa mihadarati na utovu wa usalama katika eneo hilo.
Gago amesisitiza umuhimu wa vijana kushirikiana kuleta maendeleo na kudumisha amani huku akiahidi kuendelea kukuza talanta za vijana mashinani.