Zaidi ya mahafala 200 wahitimu katika chuo cha North Coast Medical Training College

Jumla ya mahafala 202 wamefuzu katika vitengo mbalimbali katika taaluma ya utabibu na udaktari katika chuo cha North Coast Medical Training College.Licha ya changamoto ya janga la ugonjwa wa corona wanafunzi hao wamefanya vyema katika masomo mbalimbali.

Hii ni kulingana na mkuu wa maswala ya masomo na kaimu mkuu wa shule kwa sasa John Mwawana Mlugu. John amesema kutopatana na wanafunzi ana kwa ana darasani kuliathiri pakubwa shughuli ya masomo ila kama shule walihakikisha shughuli za masomo zinaendelea na wanafaidika.

John pia amewashkuru uongozi wa shule pamoja na wazazi kushirikiana kuhakikisha wanafunzi hao wanaandikisha matokeo  bora,akiwatakia kila la khei katika maisha yao mapya nje ya chuo hicho.

 

Kwa upande wake Marryan Ndambingu mkurugenzi wa chuo hicho amesema chuo hicho kina mpango wa kuanzisha kituo cha utafiti ifikapo mwaka 2022 ili kuwapatia nafasi wanafunzi katika chuo hicho kufanya utafiti na kuvumbua maradhi mbalimbali.

Aidha amewarai mahafala hao kutafuta fursa za udhamini wa kimasomo ili kujiendeleza.

 

Afisa wa afya kutoka serikali ya kaunti ya Kilifi Daktari Sultan Hubeis ambae pia alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amesema kuhitimu kwa mahafala hao kutasaidia kuziba nafasi za uchache wa maafisa wa afya ambao unashuhudiwa nchini.

Sultan ameongeza kuwa wamewafungulia milango ya kupata mafunzo kazi kwa mahafala hao kujifunza mengi kuhusu utabibu.

 

Kwa upande wao mahafala hao wameelezea kufurahishwa kwa kuhitimu kwao pamoja na kuwashkuru walimu pamoja na wazazi katika mchango wao  kufanikisha kufaulu kwao.