Kina mama wa ODM waombwa kugombania nyadhfa mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu 2022

Mwenyekiti wa chama cha ODM kaunti ya Mombasa Mohamed Khamis amewaomba kina mama katika chama cha ODM kugombania nyadhfa mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Akiongea katika kaunti ya Mombasa katika uzinduzi rasmi wa kitengo cha Warembo na Raila mwenyekiti huyo amesema kina mama pia wana haki ya kikatiba kuongoza nchi katika viti mbali mbali vya kisiasa.

Mohamed pia amezidi kusistiza kuwa kura za mchujo zitakuwa za huru na haki akiahidi kuwapigania kina mama kuhakikisha wanapata haki zao.

Aidha Mohamed amesema lengo kuu la kuundwa kwa kitengo hicho cha WAREMBO NA BABA ni kuhakikisha kinauza sera za kinara wa chama hicho Raila Odinga katika azma yake ya kuwania kiti cha urais mwaka 2022 na kukipa umaarufu chama cha ODM.

Mohamed amewahimiza wanachama wa ODM kushikana na kuonyesha umoja kuhakikisha chama kinasonga mbele kimaendeleo akiongeza kuwa ofisi yake  iko tayari kufanya kazi na mtu yoyote.

Vilevile Mohamed amemshkuru gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho katika harakati zake za kukikuza chama hicho pamoja na kuamua kisimama na Raila katika azma yake ya kugombania urais  2022 ili kuimarisha taifa la kenya kimaendeleo.

Amewarai wanachama wa ODM kuzidi kumuunga mkono Raila Odinga kwani ndie chaguo sahihi kwa wakenya na suluhu kwa shida wanazopitia.