Cheche ya Tete Pwani “Habib Swaleh Ndani ya Karne ya 21”
Mwambao wa pwani huwenda ukaimarika na kutajika tena maeneo mbali mbali ulimwenguni kama ilivyo kuwa awali kwa kuzindua historia yake ya kale iliyovuma pwani hadi bara.
Cheche inayoratajiwa kufufua mafanikio katika pwani ya Kenya inajiri baada ya uzinduzi wa filamu iliyopewa jina Tete katika ukumbi wa Alliance Francaise eneo bunge la nyali katika kaunti ya Mombasa.
Kama jina lake Tete, Filamu hii inamzungumzia mkaazi na mwanachuoni katika eneo la Lamu aliyekuja kama mgeni kutoka visiwa vya Ngazija maarufu Comoro na kisha kukita kambi eneo hilo alipoanzisha na kuendeleza mafanikio si haba.
katika uzinduzi huo viongozi mbali mbali walihudhuria ikiwemo viongozi wakidini kutoka sehemu tofauti mkoani pwani, mwakilishi wadi mteule Bi. Amina Kale, Prof. Lela kutoka chuo kikuu cha Mombasa, Gwiji wa kiswahili Rashid Abdalla pamoja na viongozi wengineo. Ujio wa viongozi hawa ukiwa ishara tosha ya utayari wa kuenzi na kukuza turathi mbali mbali zinazoenziwa mkoani na Vitongojini.
Kinyume na matarajio ya wengi filamu hii imetayarishwa na kuzinduliwa na kijana, mwana filamu na mtengenezaji maudhui Omar Swaleh Maarufu Omar Kibulanga miaka 85 baada ya kufariki kwa shujaa huyu Habib Swaleh.
Maisha ya Habib Swaleh kama yalivyoangaziwa katika filamu hii yalikuwa ya kipekee, yalio jaa uweledi wa tiba na dawa za miti shamba, busara na elimu isiokuwa na kifani yote ikiwa bahari ya faida kwa wenyeji na kusambazwa pembizoni mwa taifa hili hadi ng’ambo.
Aidha Habib Swaleh Muhusika mkuu katika filamu ya Tete alitambulika kwa ukarimu wake na kuwa mwazilishi wa tamaduni kadhaa na kuendeleza baadhi alizorithi kutoka kwa wavyele wake kama Usomaji wa maulidi miongoni mwa tamaduni nyingine .
Swali likisalia je, ni ipi faida ya kuzindua filamu hii inayoangazia historia ya kale hasaa wakati ambapo wengi wamekumbatia ulimwengu wa dijitali na Utandawazi?
Katika filamu hii wengi wanamkumbuka Habib Swaleh kama kiongozi na kinara aliye jikita katika masuala ya kuendeleza sekta ya elimu na kuimarisha tiba , hili liliwavutia wengi kutoka sehemu mbali mbali waliokuwa na uchu wa kusoma na kutaka kujikuza katika tiba.
Kando na hayo, Utu hujenga mtu na ndio kauli iliyomkuza daraja gwiji huyu wa kale kwa ukarimu wake kuwajali watu mbali mbali , waliokosa makao akiwapatia nafasi ya kujistiri ili kutimiza malengo yao ya kusaka elimu katika eneo lake.
Cheche hii imebainisha wazi kuwa ni wakati mwafaka wa kuzinduka na kusaka tamaduni na historia za kale ambazo ndio turathi za ngarama zitakazo kuza jamii na kukumbusha vizazi vijavyo kuhusu Maisha ya kale na kuwachorea taswira halisi ya vinara kama Habib Swaleh akilini mwao.
Kwa sasa changamoto kuu ikisalia kwa vijana na ambao wamejitwika udijitali maungoni kuendeleza na kukuza turathi za mababu na tamaduni kwani hauachi mbachao kwa msala upitao.