ZAIDI YA FAMILIA 800 OLD TOWN ZAFAIDIKA NA MSAADA WA CHAKULA

Zaidi ya familia 800 katika mtaa wa Old Town Kaunti ya Mombasa zimepokea msaada wa chakula kutoka kwa shirika la kijamii linalojitegemea la Kibokoni KISESHO. Shughuli ya kupeana msaada huo huratibiwa kila mwaka ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhan na hupania kupeana msaada huo kwa familia zisizojiweza ili kujikidhi kimaisha .

Kupitia kwa mwenyekiti wao Zubeir Noor Hussein ambaye pia aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa Tume ya Waqf nchini, amesema walilenga kusaidia familia Zaidi ya 1000 lakini kutokana na ujio wa corona na hali ya maisha kuwa ngumu hawakuweza kufikisha msaada wa kutoshea idadi hiyo. Zubeir amewashukuru waliofanikisha zoezi hilo na kuwaomba wazidi kushirikiana katika miradi mengine ya kijamii.

Zubeir amesema shughuli hyo pia imezingatia kanuni za corona kwani walengwa wamapelekewa chakula hadi nyumbni kwao ili kuepuka watu kukongamana pamoja na kujiweka katika hatari ya kupata corona.

 

Vilevile Zubeir amesema wamekuwa mstari wa mbele kuwawezesha jamii kupitia miradi mbalimbali kama michezo,elimu na miradi ya kina mama huku akiahidi kutafuta muafaka wa swala la utovi wa usalama katika mtaa huo kwa kushirikiana na idara za usalama,washikadau mbalimbali pamoja na jamii.

 

 

Kwa upande wake mwenyekiti wa shirika la msalaba mwekundi kaunti ya Msa Mahmoud Noor amepongeza mradi huo na  kuwarai wadhamini Zaidi kujitokeza kufadhili shughuli hiyo haswa katika kipindi hiki cha corona ambapo familia nyingi zimekumbwa na umaskini. Mahmoud pia amependekeza kuwepo kwa vituo vya mafunzo ili kuwaelekeza vijana na kuwaepusha kujiunga na makundi yasiyo na faida.

 

Abdallah Nassir ambae ni mwakilishi wa vijana pia muweka hazina katika shirika hilo la KISESHO amewasihi vijana kutotumiwa na wanasiasa pia kuepuka makundi yasiyo na faida kwao badala yake kujiunga na makundi ya kijamii yaliyo na malengo ya Umma.