Shule ya msingi ya Anfaal yatoa matokeo bora Kaunti ya Mombasa

Vifijo na nderemo zinaendelea kurindima katika shule mbali mbali kaunti ya Mombasa kufuatia matokeo ya mtihani wa kitaifa KCPE.

Katika shule ya msingi ya kibinafsi ya Anfaal huko Nyali Kaunti ya Mombasa imeorodhesha matokeo bora ya KCPE 2020 na kuandikisha jumla ya alama ya wastani ya 366, huku mwanafunzi bora Abdullatif Abdurashid akiibuka na alama 388.

Sheikh Hassan Sugow ambaye ni msimamizi wa shule hiyo ameeleza kuridhishwa na matokeo hayo ikikumbukwa kuwa ni mwaka wao wa kwanza kufanya mtihani wa kitaifa KCPE.

 

Sumeiya Suo ni miongoni mwa wanafunzi waliotia fora katika mtihani wa KCPE ambapo Abdullatif Abdurashid aliongoza kwa alama 388 akifuatiwa na Mohammed Abdulshakur kwa alama 386, na anasema kuwa msaada wa walimu wao na juhudi zao zimepelekea wao kufaulu.

Kwa upande wake naibu mwalimu mkuu wa shule hiyo Said Baya amekiri kuwa ujio wa Corona ulitatiza shughuli na hata kulazimika kubadili mbinu za masomo na sasa anabaini kuwa tayari wameanza mikakati kabambe ya masomo kabla muhula ujao ili waimarishe matokeo bora zaidi.

Kwengineko msichana Maua Omar Salim kutoka shule ya kibinafsi ya Anwar huko Mshomoroni eneo bunge la Kisauni amewapiku na kuwabwaga wavulana kwa kuzoa alama 385 na kuongoza shuleni humo akifuatiwa kwa karibu na Abubakar Abdalla kwa alama 380.